RUCU MAMBO NI SWARI
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mh. Kheri James, leo amefanya ziara Chuoni (RUCU) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yaliyotangaza kufunguliwa kwa vyuo vikuu kuanzia tarehe 17 Novemba 2025.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alipokelewa na mwenyeji wake, Makamu Mkuu wa Chuo, Sr. Prof. Lekule, ambaye aliwasilisha mpango kazi wa maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wapya, wanaoendelea pamoja na maandalizi ya Mahafali ya 18 ya chuo, yanayotarajiwa kufanyika Ijumaa, tarehe 21 Novemba 2025.
Sr. Prof. Lekule aliwasilisha taarifa inayoonyesha hatua madhubuti zilizochukuliwa na chuo kuhakikisha wanafunzi wapya wanaanza masomo katika mazingira bora, salama na yenye utulivu. Taarifa hiyo pia ilionyesha maandalizi ya sherehe za mahafali yanavyoratibiwa kuhakikisha inakuwa ya mafanikio kwa wahitimu wa mwaka 2025. Ameeleza kuwa maandalizi yote yanafanyika kwa ushirikiano wa karibu na serikali ya mkoa na Vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa, Mh. Kheri James ameipongeza RUCU kwa kuwa mbele ya muda katika kuhakikisha maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha juu.
“Hongera sana Sr. Prof. Lekule na timu yako. Nimeridhishwa na kiwango cha maandalizi ya mapokezi, weledi, ushirikiano na utayari.
RUCU imeendelea kuthibitisha ubora kwa Mkoa wetu kama kitovu cha elimu bora nchini,” amesema Mh. Mkuu wa Mkoa.
Ameongeza kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na uongozi wa chuo katika kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa salama, swari na tulivu kwa Jumuiya yote ya RUCU na wageni.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo alitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa kwa kutenga muda kutembelea chuo na kuendelea kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya elimu mkoani Iringa. Sr. Prof. Lekule pia alitumia nafasi hiyo kumkaribisha rasmi Mkuu wa Mkoa katika Mahafali ya 18 ya RUCU yatakayofanyika tarehe 21 Novemba 2025.
Source: PRO's Office